Mikabala Ya Uandishi Wa Vitabu Vya Kiada Na Mchango Wake Katika Ufundishaji Na Ujifundishaji Wa Mtindo Wa Insha Katika Shule Za Upili Nchini Kenya

Thesis tittle: Mikabala Ya Uandishi Wa Vitabu Vya Kiada Na Mchango Wake Katika Ufundishaji Na Ujifundishaji Wa Mtindo Wa Insha Katika Shule Za Upili Nchini Kenya

Students’ name: Ateya Nester

Supervisors:

  1. Eric W. Wamalwa
  2. Stanley A. Kevogo

 

IKISIRI

Vitabu vya kiada vina nafasi kubwa katika ufundishaji na ujifundishaji wa insha za Kiswahili katika shule za upili nchini Kenya. Licha ya umuhimu huu katika mchakato wa ufundishaji na ujifundishaji, vitabu vya kiada huwasilisha mikabala tofauti kuhusu mtindo wa insha na hivyo, kuwatatiza walimu na wanafunzi wanaovitumia. Utafiti huu ulilenga kuchunguza mikabala ya uandishi wa vitabu vya kiada na mchango wake kwa ufundishaji na ujifundishaji wa mtindo wa insha za Kiswahili. Utafiti uliongozwa na madhumuni mahsusi yafuatayo: Kwanza, kubainisha mikabala mbalimbali ya waandishi wa vitabu vya kiada kuhusu ufundishaji na ujifindishaji wa mtindo wa insha. Pili, kudadavua athari za matumizi ya vitabu tofauti vya kiada katika ufundishaji na ujifundishaji wa mtindo wa insha. Tatu, kutathmini matumizi ya vitabu vya kiada katika ufundishaji na ujifundishaji wa insha katika shule za upili. Mseto wa nadharia mbili ulitumika. Nadharia ya Mtindo iliyoasisiwa na Milic Louis (1965) kwa kuzingatia mihimili ya ubinafsi na muundo; na Nadharia ya Umaizi Mwingi ya Howard Gardner (2000) kwa kurejelea mihimili ya utambulisho, uimarishaji na uainishaji. Mkabala wa utafiti ulikuwa wa mseto, muundo ukiwa wa kimaelezo. Utafiti ulifanywa katika eneo la Kaunti ndogo ya Mumias Magharibi, Kaunti ya Kakamega. Utafiti uliwalenga walimu wa Kiswahili na wanafunzi wote wa kidato cha kwanza hadi cha nne wa shule za upili kaunti ndogo ya Mumias Magharibi. Sampuli ya utafiti iliteuliwa kitabakishi, kimaksudi na kinasibu. Walimu 22 na wanafunzi 320 walishirikishwa. Data ilikusanywa kupitia mbinu ya uchanganuzi wa yaliyomo, hojaji na usaili. Zana za ukusanyaji wa data zilijumuisha kielelezo cha uchanganuzi wa nyaraka, mwongozo wa usaili na dodoso. Data ya kiidadi ilichanganuliwa kitakwimu na kuwasilishwa kwa majedwali na maelezo. Data ya kithamano ilichanganuliwa kupitia njia ya uchanganuzi wa yaliyomo na imewasilishwa kimaelezo. Matokeo ya utafiti yamebainisha kwamba vitabu vya kiada vinaibua mikabala tofauti miongoni mwa walimu na wanafunzi kuhusu mtindo wa uandishi wa insha katika shule za upili. Pili, matumizi ya vitabu tofauti vya kiada yana athari chanya kwa wanafunzi wa uwezo wa kadri na juu wa kielimu na hasi kwa wale wa uwezo wa chini wa kielimu katika ufundishaji na ujifundishaji wa mtindo wa insha katika shule za upili. Matokeo yalionesha kwamba vitabu tofauti vya kiada havijachangia ipasavyo katika kuimarisha ufundishaji na ujifundishaji wa insha za Kiswahili ka.tika shule za upili eneo la Mumias Magharibi, ingawa tathmini ya matumizi ya vitabu tofauti vya kiada katika ufundishaji kwa ujumla ilibaini kuwa vitabu vya kiada vina mchango mkubwa katika kuimarisha na kuendeleza ufundishaji na ujifundishaji wa insha. Matokeo ya utafiti huu yanatarajiwa kuwafaidi wanafunzi na walimu wa Kiswahili katika shule za upili na viwango vingine vya elimu nchini Kenya kwa kupanua maarifa na ujuzi wao kuhusu mtindo wa uandishi wa insha. Isitoshe, wakuza mitaala na waandishi wa vitabu vya kiada vya Kiswahili huenda wakafaidi kutokana na mapendekezo ya jinsi ya kuimarisha uandishi na matumizi ya vitabu vya kiada. Utafiti huu umependekeza kwamba walimu na wanafunzi wapewe fursa na kuhusishwa katika uchaguzi na matumizi ya vitabu tofauti vya kiada vinavyokidhi mahitaji yao.