Thesis Title: Mchango wa Mofofonolojia ya Kiduruma katika Ujifunzaji wa Sarufi ya Kiswahili: Mfano wa Shule za Msingi katika Kaunti ya Kwale, Kenya.
Student’s Name: Noah Munda Majele
Supervisors:
Ikisiri
Ingawa kuna tafiti nyingi ambazo zimefanywa kuhusu mofofonolojia ya lugha mbalimbali, tafiti hizo zimechambua, kuchanganua mifanyiko na kulinganisha mofofonolojia ya lugha moja na nyingine bila kuzingatia mchango wa mofofonolojia ya lugha moja kwa lugha nyingine. Utafiti huu ulipambanua mchango wa mofofonolojia ya Kiduruma kwa ujifunzaji wa sarufi ya Kiswahili kwa shule za msingi katika kaunti ya Kwale. Utafiti uliongozwa na madhumuni manne: Kwanza, kubainisha uhusiano wa mofofonolojia ya Kiduruma na ya Kiswahili. Pili, kulinganisha mifanyiko ya mofofonolojia katika Kiduruma na ile ya Kiswahili. Tatu, kufafanua matokeo ya uhusiano wa mofofonolojia ya Kiduruma na ya Kiswahili. Nne, kupambanua mchango wa mofofonolojia ya Kiduruma katika ujifunzaji wa sarufi ya Kiswahili. Utafiti uliongozwa na nadharia ya Fonolojia Zalishi Asilia ambayo iliasisiwa na Joan Hooper (1971) pamoja na nadharia ya Ujifunzaji Lugha kwa Vitendo (ULUVI). Utafiti ulitumia mkabala wa kithamano ambao unatumia maelezo. Kwa kuwa utafiti unahusu lugha, ulitumia muundo wa kiethinografia. Utafiti uliwalenga wanafunzi wa gredi ya tano wa shule za msingi za umma katika kaunti ya Kwale. Sampuli ya wanafunzi 357 iliteuliwa kwa usamplishaji nasibu. Data ilikusanywa kutumia mbinu ya uandishi wa insha. Data ilichanganuliwa kwa njia ya uchanganuzi wa yaliyomo na kuwasilishwa kwa kutumia majedwali, michoro na maelezo. Matokeo ya utafiti yalionesha kuwa kuna uhusiano katika mofofonolojia ya Kiduruma na Kiswahili kupitia miundo ya silabi, fonimu, ngeli, njeo na mnyambuliko wa maneno. Ilibainika kuwa kuna mfanano katika mifanyiko ya mofofonolojia ya Kiswahili na Kiduruma. Uhusiano huo ulitokana na athari kama vile ukopaji wa maneno, mabadiliko ya kisarufi, uchopekaji, ubadala wa fonimu na udondoshaji wa fonimu. Kutokana na uhusiano huu, utafiti umehitimisha kwamba mofofonolojia ya Kiduruma huenda ikawa na nafasi katika ujifunzaji wa sarufi ya Kiswahili kupitia kuoanisha fonimu za Kiswahili na Kiduruma, miundo ya silabi, ngeli, nyakati mbalimbali na mnyambuliko wa maneno.
Postal Address:
P.O. Box 1699-50200
BUNGOMA – KENYA
Telephone Number: +254708085934
Email: sgs@kibu.ac.ke