Utafiti ulichunguza matumizi ya vifaa vya kisasa katika ufundishaji na ujifunzaji wa sarufi katika shule za upili zilizoko kaunti ndogo ya Moiben. Malengo ya utafiti yalikuwa ni: Kuthibitisha upatikanaji wa vifaa vya kisasa, kuchunguza jinsi walimu hutumia vifaa vya kisasa katika kufundisha sarufi, kuhakiki umuhimu wa matumizi ya vifaa vya kisasa katika ufundishaji na ujifunzaji wa sarufi. Utafiti ulifanyika katika kaunti ndogo ya Moiben iliyoko katika kaunti ya Uasin Gishu. Eneo hili lilichaguliwa kimakusudi kuwakilisha maeneo mengine nchini Kenya yenye sifa sawa za ufundishaji na ujifunzaji. Utafiti uliongozwa na nadharia ya kujifunza kiugunduzi yake Bruner (1966). Utafiti ulizingatia muundo wa utafiti kimfano. Ulilenga shule za upili kumi na tano kati ya ishirini na sita zilizoko katika kaunti ndogo ya Moiben. Walengwa walikuwa walimu kumi na watano wanaofundisha sarufi na wanafunzi mia moja na watano wa kidato cha tatu. Walimu walichaguliwa kwa kuzingatia vipindi vya sarufi ya Kiswahili wanavyovifundisha. Wanafunzi wa kidato cha tatu walihusishwa kwa kuwa mada zilizolengwa katika utafiti zilifundishwa katika kidato cha tatu. Hojaji, mahojiano na uchunzaji zilitumika kukusanya data. Uchunzaji ulitumika kupata data kuhusu vifaa vinavyotumika darasani kufundisha sarufi. Hojaji ya mwalimu na mwanafunzi ilitumika kupata data kuhusu umuhimu wa matumizi ya vifaa vya kisasa katika ufundishaji na ujifunzaji wa sarufi. Mahojiano yalitumika kupata data kuhusu changamoto za matumizi ya vifaa vya kisasa. Data iliyokusanywa iliwasilishwa kwa kutumia asilimia majedwali. Hatimaye, data hii ilichanganuliwa kimaelezo. Matokeo ya utafiti yalibaini kuwa, chini ya asilimia 20 ya walimu katika kaunti ndogo ya Moiben walitumia tarakilishi na vipakatalishi pamoja na vinuruweo katika ufundishaji na ujifunzaji wa sarufi. Matokeo yalithibitisha kuwa, vifaa hivi hurahisisha uelewekaji wa mada za sarufi, huleta uchangamfu darasani, huokoa muda na kuwashirikisha wanafunzi katika somo. Matumizi ya vifaa hivi yanakumbwa na changamoto kama vile: ukosefu wa mtandao shuleni, idadi kubwa ya wanafunzi, hitilafu za umeme, upungufu wa fedha za kuvinunua vifaa hivi, upungufu wa wakati na upungufu wa ujuzi wa matumizi baina ya walimu. Matokeo ya utafiti huu yatakuwa ya manufaa kwa wizara ya Elimu nchini Kenya. Kutokana na changamoto zinazokumba matumizi ya vifaa vya kisasa, matokeo haya yanaweza yakaisaidia Wizara ya Elimu kubuni mikakati ya kuzikabili changamoto hizi na kuyaboresha matumizi ya vifaa hivi. Aidha, yatawanufaisha walimu wa shule za upili kwa kuwa yatatoa fahamu zaidi kuhusu matumizi ya vifaa vya kisasa katika ufundishaji na ujifunzaji wa sarufi.

Author: Joachim, Melly Kipchirchir
Year: 2019